Alhamisi 27 Agosti 2026 - 16:50
Hawzah na Urithi wa Kihistoria wa “Maktaba ya Shahidi Nasrullah”: Kutoka Kufafanua Jukumu la Kihawza Hadi Kuandaa Mikakati ya Kiutendaji

Hawza/ Katika kikao maalumu imefafanuliwa kuhusu Maktaba ya Shahidi Nasrullah”: Kutoka Kufafanua Jukumu la Kihawza Hadi Kuandaa Mikakati ya Kiutendaji

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, mkutano wa kielimu na kitaalamu wenye mada “Hawzah na Majukumu Yanayotokana na Ujumbe wa Imam wetu Shahidi; kwa Kuwasilisha Njia ya Maktaba ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah” umefanyika katika Madrasa ya Ayatollah Eirvani, kwa uenyeji na ushirikiano wa pamoja kati ya Sekretarieti ya Kimataifa ya Umana al-Rusul na Uongozi wa hawzah ya Wanawake.

Mkutano huo ulikuwa ni juhudi za kiakili za kutathmini upya nafasi ya vyuo vya dini katika mfumo wa kistaarabu wa Uislamu na kuchunguza mwenendo wa kiuongozi wa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kama mfano wa kistaarabu na wa kisasa.

Katika mkutano huo, Hujjat al-Islam wal-Muslimin Muhammad-Taqi Rabbani, Katibu wa Kamati ya Kielimu ya Sekretarieti ya Umana al-Rusul, alifafanua kwa mtazamo wa kiuchambuzi uhusiano kati ya hawzah, jukumu la kihistoria la wanazuoni wa dini na mfumo wa utendaji wa Shahidi Nasrullah.

Hawzah; mwendelezo wa Shule ya Uimamu

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani, mwanzoni mwa hotuba yake, kwa kurejea chimbuko la kihistoria la hawzahi, alikitaja chombo hiki si kama taasisi ya elimu pekee, bali kama mwendelezo wa mkondo halisi wa “Shule ya Uimamu.”

Akirejelea matukio yaliyotokea baada ya Ashura, alisema: “Baada ya tukio hili, Imam Sajjad (as), kwa kuchora mstari sambamba dhidi ya ‘Shule ya Ukhalifa’ — ambayo inajulikana kwa jina la Saqifah — aliweka msingi wa kurejesha utambulisho wa Kishia.”

Kwa mujibu wake, jukumu la shule hii lilikuwa kulinda fikra safi; na kwa kuwa kipindi hicho kilikuwa miongoni mwa vipindi vya ukandamizaji mkubwa, hawzah za leo pia zinapaswa kufahamu kwamba jukumu lao si kuhamisha maarifa ya kimaandishi pekee, bali zina jukumu pana zaidi linalojengwa juu ya dhana mbili muhimu za “kuonya” na “kuwasaidia na kuwaokoa.”

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani aliongeza: “Jukumu hili ni mwamko wa Mwenyezi Mungu unaoiondoa jamii katika hali ya kutokuwa na mwitikio na kuipeleka kuelekea kilele cha ukamilifu wa kistaarabu.”

Hawzah za wanawake; jambo la kistaarabu

Mzungumzaji wa mkutano huo, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizingatia uwezo mpya wa kihawza, alisema kuanzishwa kwa vyuo vya dini vya wanawake ni miongoni mwa baraka kubwa za Mapinduzi ya Kiislamu na ni “jambo kubwa la kistaarabu.”

Alisisitiza: “Hawzah za wanawake si maeneo ya elimu pekee, bali ni taasisi za kuwaandaa watu wanaoongoza na kusukuma mbele maendeleo ya kijamii.”

Mwalimu huyo wa hawzah alijikita kwenye nyanja mbili muhimu za nafasi ya wanafunzi wanawake wa vyuo vya dini: kwanza, usimamizi wa uwanja wa familia, na pili, kutekeleza jukumu katika ufafanuzi wa masuala makubwa ya kijamii.

Alisema nafasi ya wanafunzi wanawake wa hawzah katika kukabiliana na changamoto za kifikra na kiutamaduni za leo ni jambo lisiloweza kupingika, na akaongeza: “Taasisi hii inaweza kuwa kama mkono wenye nguvu wa kuujenga upya utambulisho wa Kiislamu na kutekeleza nafasi ya kimkakati katika jamii.”

Uchambuzi wa mradi wa “Istikhfaf” kwa mujibu wa mantiki ya Qur’ani

Miongoni mwa mihimili mikuu ya hotuba ya Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani ilikuwa uchambuzi wa mradi wa kimkakati wa tawala za kitaghuti wa kuitawala jamii; mradi ambao aliuita “Istikhfaf” — yaani kuwafanya watu kuwa wanyonge, kuwadharau na kuwafanya wajione kuwa hawana thamani.

Akitumia mantiki ya Qur’ani kuhusu namna Firauni alivyolishughulikia taifa lake, alirejelea aya isemayo:

«فَاسْتَخَفَّ قَوْمَهُ فَأَطَاعُوهُ»

“Basi aliwadhalilisha na kuwafanya watu wake kuwa wepesi wa akili, nao wakamtii.”

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani alisisitiza: “Mifumo ya kitaghuti katika historia yote imetumia njia moja ya kutawala; njia inayojengwa juu ya kuwadharau watu, kuwafanya waonekane wadogo na kuwanyang’anya heshima na utu wao.”

Aliendelea kusema: “Mradi huu uliendelea baada ya Saqifah, katika kipindi cha tawala za Banu Umayyah na Banu Abbas, na pia katika zama za kisasa kwa sura mpya kupitia ukoloni wa kisasa, ili kuufanya Umma wa Kiislamu kuugua ugonjwa wa kukubali udhalili na kujiona kuwa duni.”

Mapinduzi ya Kiislamu na kurejea heshima ya Kiislamu

Katibu wa Kamati ya Kielimu ya Sekretarieti ya Umana al-Rusul aliendelea kusema kwamba; Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa sababu ya kuvunjwa kizuizi cha udhalilishaji wa kihistoria na kuweka mazingira ya kurejea heshima ya Kiislamu.

Alisema: “Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kusimama dhidi ya mchakato wa kihistoria wa kuidhalilisha na kuinyang’anya utambulisho jamii ya Kiislamu, na kufungua njia ya kurejea heshima ya kidini na kijamii.”

Kwa mujibu wa Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah aliifanya heshima hii ionekane katika uwanja wa kimataifa na katika kukabiliana na maadui wakali zaidi wa mwanadamu, na akaonesha kwamba inawezekana, kwa kutegemea misingi ya kidini, kuibadilisha jamii iliyokuwa chini ya shinikizo na kunyimwa haki kuwa nguvu yenye uwezo mkubwa na wa kuzuia mashambulizi.

Shahidi Nasrullah; shule ya kiuongozi na kistaarabu

Mzungumzaji wa mkutano huo aliendelea kwa kueleza sifa za utu wa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, akimtambulisha si kama mtu binafsi tu, bali kama “shule ya kiuongozi na kistaarabu.”

Miongoni mwa sifa kuu za shule hii alizitaja kuwa ni: akili pana na uwezo mkubwa wa kufikiri; usimamizi wa migogoro; uwezo wa kujenga maridhiano na kutatua migongano; pamoja na uwezo wa kuleta mshikamano kati ya makundi mbalimbali ya kijamii.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kielimu ya Mahdawiyyah ya Vyuo vya Dini, huku akirejelea muundo tata wa kijamii wa Lebanon, alisema: “Shahidi Nasrullah aliweza kubadilisha mipasuko mikubwa iliyokuwapo kati ya makundi mbalimbali ya Walebanon, wakiwemo Mashia, Masunni, Druze na Wakristo, kuwa mshikamano katika njia ya Muqawama.”

Alisema; uwezo huu ni miongoni mwa dhihirisho muhimu la shule ya kiuongozi na kistaarabu ya Shahidi Nasrullah, na akasisitiza: “Usimamizi wa jamii yenye makundi mbalimbali unahitaji uelewa sahihi wa kijamii, uwezo wa kufanya mazungumzo, kushawishi na kujenga imani miongoni mwa makundi mbalimbali.”

Kuwapa heshima wanyonge na kubadilisha unyonge kuwa nguvu

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani, katika sehemu nyingine ya uchambuzi wake, alizungumzia nafasi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasralluh katika kuwapa heshima maskini na jamii yenye kunyimwa zaidi Lebanon.

Alisema: “Shahidi Nasrullah aliweza kuibadilisha jamii iliyokuwa katika hali ya kunyimwa nguvu na kudhoofishwa kuwa nguvu yenye uwezo mkubwa na yenye uwezo wa kuzuia mashambulizi.”

Kwa mtazamo wake, mabadiliko haya ya kijamii ni somo kubwa zaidi kwa watu wa hawzah; kwa sababu yanaonyesha jinsi inavyowezekana, kwa kutegemea misingi ya kidini, kuamsha uwezo wa kijamii wa watu wanyonge na kuifikisha jamii dhaifu na iliyokuwa chini ya shinikizo kuwa nguvu yenye ushawishi na yenye uwezo wa kuamua mambo.

Ulazima wa kuvuka hatua ya kumuenzi kwa hisia

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Rabbani, katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, alitaka kuwe na kuvuka kutoka katika “kumuenzi kwa hisia” na kuingia katika uwanja wa “kuandaa mbinu na mifumo.”

Akikosoa kujitosheleza kwa kusifu na kumuenzi mtu wakati wa kushughulikia shakhsia za kistaarabu, alisema: “Jukumu la hawzah si kuwaheshimu tu watu kama Shahidi Nasrullah, bali inapaswa, kutokana na mwenendo na uzoefu wao, kutoa ‘kitabu cha kazi’ na ‘maelekezo ya kiutendaji.’”

Alipendekeza kwamba watafiti na vituo vya kielimu wageuze vipengele mbalimbali vya mwenendo wa Shahidi Nasrullah kuwa mifumo ya kielimu na mafunzo, ikiwemo:

1- Mbinu na ujuzi wa kumshawishi msikilizaji;

2- Mifumo ya usimamizi wa migogoro katika jamii zenye makabila na madhehebu mbalimbali;

3- Misingi ya kuishi na kufanya shughuli kwa ufanisi katika mazingira yenye hatari na vikwazo vingi;

4- Sanaa na mbinu za operesheni za vyombo vya habari.

Kwa mujibu wake, mihimili hii inaweza kuweka mazingira ya kuandaliwa kwa mfumo wa kielimu wa kuwafundisha watu wanaoshughulika katika nyanja za kijamii, kiutamaduni na kihawzah.

Kujenga uwezo wa kistaarabu kwa ajili ya maandalizi ya kudhihiri

Katibu wa Baraza la Kielimu la Sekretarieti ya Umana al-Rusul, mwishoni, aliichukulia harakati hii ya kielimu na kiutafiti kuwa utangulizi muhimu wa kujenga uwezo katika njia ya maandalizi ya kweli ya kudhihiri Imam wa Zama, Walii wa Mwenyezi Mungu, (aj).

Alisisitiza: “Kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu kunahitaji kujengwa kwa uwezo halisi na wa kistaarabu miongoni mwa wanaosubiri. Kusubiri hakutimizwi kwa kutoa kauli mbiu au kuonesha mapenzi pekee; bali kunapaswa kubadilishwa kuwa uwezo wa kijamii, kifikra, kiuongozi na wa kistaarabu.”

Mkutano huo ulihitimishwa kwa kusisitiza ulazima wa kuendelezwa ushirikiano wa pamoja kati ya taasisi za kielimu na za uenezaji wa maarifa, pamoja na kuendelezwa tafiti kuhusu “Maktaba ya Muqawama.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha